16 Desemba 2020 - 12:36
Human Rights Watch: Mamia ya wafungwa wa Kiafrika wapo katika mazingira mabaya Saudia

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, kuna mamia ya vibarua na wahajiri wa kigeni wanaoteseka katika magereza ya Saudi Arabia kutokana na mazingira mabaya katika magereza hayo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa ya shirika hilo imeeleza kuwa,  wafungwa hao ambao ni raia wa Kiafrika mbali na mazingira mabaya wanayokabaliana nayo katika magereza hayo pia wamekuwa wakifanyiwa miamala na vitendo visivyo vya kibinadamu.

Baadhi ya wafungwa walioachiliwa huru wamesimulia kwamba, wafungwa wa Kiafrika katika magereza hayo wamekuwa wakiteswa na kufanyiwa vitendo visivyo vya kibinadamu na kwamba, kuanzia mwerzo Oktoba hadi sasa kuna wenzao watatu ambao wameaga duniani gerezani kutokana na mateso.

Sehemu nyingine ya ripoti ya Human Rights Watch inasema, maelfu ya wahajiri hao wa Kiethiopia wanapitia kipindi kigumu katika vituo vya kuwazuilia nchini Saudia, na hali imekuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki cha janga la corona.

Hivi karibuni pia, Human Rights Watch iliripoti kuwa makumi ya wahajiri wa Kiethiopia waliokimbia vita kaskazini mwa Yemen wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa mpakani wa Saudi Arabia.

Ethiopia inakadiria kuwa makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wanaofanyakazi nchini Saudi Arabia wako chini ya mashinikizo makubwa na wengi miongoni mwao wamekwama hapo bila kazi wala kipato.

Shirika hilo mara kadhaa limeutaka Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kusitisha mateso ya wahajiri hao wa Kiethiopia nchini Saudi Arabia na kuwachukulia hatua wahalifu waliohusika na mauaji ya makumi ya wahajiri hao na ukiukaji mwingine wa haki zao.

342/